Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ limeweka wazi Ratiba ya Ngao ya Jamii mwaka 2023 kwa kushirikisha timu nne zilizomaliza nafasi za nne juu katika Msimamo wa Ligi Kuu msimu uliopita 2023/24.
Kwa mara ya kwanza TFF imetangaza mfumo huo baada ya kufanywa kwa mabadiliko kanuni za mchezo wa Ngao ya Jamii, ambapo awali ulikuwa unashirikisha timu mbili, (Bingwa wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara/ Bingwa wa Ligi Kuu dhidi ya Mshindi wa Pili wa Ligi Kuu.).
Leo Jumamosi (Julai 08) TFF imetangaza Ratiba ya michuano ya Ngao ya Jamii ambayo itafanyika jijini Tanga katika Uwanja wa CCM Mkwakwani mapema mwezi Agosti.
Mchezo wa kwanza utashuhudia Mabingwa wa Tanzania Bara Young Africans Young Africans wakicheza dhidi ya Azam FC iliyomaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu msimu wa 2022/23.
Mchezo huo wa kwanza umepangwa kuchezwa Agosti 09 saa moja usiku.
Mchezo wa pili wa Michuano hiyo utazikutanisha Simba SC iliyomaliza nafasi ya Pili dhidi ya Singida Fountain Gate iliyomaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu msimu wa 2022/23.
Mchezo huo umepangwa kupigwa Agosti 10 saa moja usiku.
Mshindi wa mchezo wa kwanza atakutana na mshindi wa mchezo wa Pili katika hatua ya Fainali itakayopigwa katika Uwanja wa CCM Mkwakwani Agosti 13 saa moja usiku. Mchezo wa kumsaka Mshindi watatu na wanne utatangulia siku hiyo (Agosti 13) majira ya saa tisa alasiri, kwa kuzikutanisha timu zilizopoteza mchezo wa kwanza na wa pili.