Kocha Mkuu wa Simba SC Robert Oliviera ‘Robertinho amemuhakikishia nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, Kiungo kutoka DR Congo Fabrice Ngoma huku vita akacha kwa nyota wake wawili.
Awali Mkongomani huyo wakati anajiunga na timu hiyo, akitokea Al Hilal ya nchini Sudan hakuwa katika kikosi cha kwanza huku akijikuta akisugua benchi katika michezo ya mwanzoni.
Kiungo huyo alikuwa akisoteshwa benchi na nyota Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute kabla ya hivi sasa kuaminika na kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Simba SC, rasmi Ngoma amejihakikishia nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, huku akiwaachia vita ya kugombania nafasi moja ya kiungo ambao ni Mzamiru na Kanoute.
Mtoa taarifa huyo amesema kati ya Mzamiru na Kanoute ndio watakaopishana kucheza namba 8, ambao katika michezo ya Ligi Kuu Bara na African Football League wameonekana kubadilishana.
Ameongeza kuwa, Ngoma yeye uhakika ataanza kucheza namba 6,ni baada ya Robertinho kuvutiwa na aina yake ya uchezaji kupiga pasi, kupunguza mashambulizi na kutuliza timu wakati ikishambuliwa.
“Ngoma amelivutia benchi la ufundi kutokana na aina yake ya uchezaji, hiyo imemfanya aingie moja kwa moja katika kikosi cha kwanza kutokana na kuwazidi wachezaji aliowakuta Mzamiru na Kanoute.
“Hivi sasa Mzamiru na Kanoute watakuwa wanapishana kucheza namba 8 na kumuachia 6 Ngoma katika michezo ijayo ya ligi na kimataifa.
Licha ya Ngoma kuhakikishiwa nafasi hiyo ya kucheza katika kikosi cha kwanza, lakini kocha amewataka akina Mzamiru na Kanoute kuonyesha viwango bora vitakavyowaingiza katika kikosi cha kwanza moja kwa moja,” amesema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo, Robertinho amesema kuwa: Wachezaji wangu wote wana nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza, kikubwa ninataka kuona mchezaji aliyekuwepo uwanjani ana kiwango sawa na yule aliyekaa benchi.
Mfano mchezo wa kwanza wa African Footbal League, tulipocheza dhidi ya Al Ahly, Baleke (Jeane) na Kanoute walitokea benchi na kubadili mchezo na kufanikiwa kupata mabao mawili, hivi ndio ninavyotaka kuona katika timu.”