Ng’ombe wa maziwa wamesafirishwa kwa ndege kutoka Ujerumani kwenda Qatar kwaajili ya kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini humo wakati taifa hilo likiendelea kutengwa na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Ng’ombe 165 wa maziwa aina ya Holstein wamewasili nchini Qatar kutoka Ujerumani ikiwa ni awamu ya kwanza huku ng’ombe wengine 4000 wakitarajiwa kusafirishwa kwenda katika nchi hiyo.
Qatar imekuwa katika mgogoro mkubwa na nchi zinazounda umoja wa Falme za Kiarabu, huku vikwazo mbalimbali ikiwekewa na nchi hizo vikiwemo vya kutoshirikiana katika masuala mbalimbali kama usafiri wa anga, baharini na nchi kavu.
Aidha, kundi la nchi za Kiarabu ambazo zimeiwekea vikwazo nchi hiyo kwa tuhuma za kufadhili makundi ya kigaidi ambayo yamekuwa yakitishia amani katika eneo hilo zinaongozwa na Saud Arabia ambayo imetishia kuchukua hatua kali dhidi ya Qatar endapo haitatimiza masharti iliyowekewa.
Hata, hivyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Power International, Moutaz aL Khayyat amesema kuwa ng’ombe hao tayari wameshawasili na kwa ndege ya mizigo ya Qatar Airways na kupelekwa sehemu maalumu ya walikoandaliwa.