Benchi la Ufundi na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania Bara chini ya Umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes wamesema kesho Alhamisi watapambana kupata alama tatu dhidi ya ndugu zao wa Zanzibar ili kumaliza kileleni mwa msimamo wa Kundi B la michuano ya CECAFA U20 Chalenji Cup inayoendelea nchini Uganda.

Tanzania Bara tayari imekusanya alama nne katika mechi mbili za mwanzo na kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, wakati Zanzibar inahitaji kupata angalau alama moja kwenye mchezo huo ili kutinga hatua hiyo ya robo fainali.

Hata hivyo endapo Ethiopia itashindwa kupata ushindi dhidi ya Kenya, Zanzibar itafuzu robo fainali pia.

Kiungo wa timu hiyo, Novatus Dismas amesisitiza kuwa wanafahamu kuwa Zanzibar itakamia mchezo huo ili kupata tiketi ya kufuzu robo fainali, lakini wao wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi ili kumaliza kama vinara wa kundi.

“Tumewaona Zanzibar wanavyocheza, itakuwa mechi ngumu. Hata hivyo kama wachezaji tumejipanga vizuri, tunataka kumaliza kama vinara wa kundi maana hatujui tutakutana na nani kwenye hatua inayofuata,” alisema Dismas anayeichezea Biashara ya Mara kwa mkopo akitokea Azam FC.

Kwa upande wake kocha Mkuu, Zuberi Katwila, amesema anafahamu ushindani uliopo baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, hivyo amewaandaa vijana wake kiufundi kuhakikisha wanacheza vizuri na kupata matokeo ya ushindi katika mchezo huo.

“Siwezi kusema nitatumia mbinu gani kuweza kupata ushindi, ila tayari tumewaona Zanzibar na nimeshawaambia wachezaji wangu kitu cha kufanya.

Licha ya kwamba Zanzibar inaweza kuwa imefahamu hatma yake kama imefuzu au la baada ya mechi ya kwanza ya Kenya na Ethiopia, bado msisimko utakuwa mkubwa,” alisisitiza kocha huyo.

Wakati huo huo, golikipa namba moja wa timu hiyo, Ally Salim amepewa mapumziko ya siku tatu baada ya kupata majeraha madogo ya bega kwenye mechi iliyopita dhidi ya Kenya.

Daktari wa Ngorongoro Heroes, Sheik Ngazija alisema; “Ally (Salim) alipata majeraha madogo kwenye mchezo dhidi ya Kenya. Tumemfanyia vipimo vya X-Rays na imeonekana ana uvimbe kidogo hivyo tumempa mapumziko ya siku tatu, baada ya hapo tutamtazama kama anaweza kuanza mazoezi.”

 

IMEANDALIWA NA GIFT MACHA

AFISA HABARI NGORONGORO HEROES

CECAFA U20 UGANDA 2019

Video: Wananchi wa Mikocheni wafunguka waliyofanyiwa na viongozi wa serikali ya mtaa
Toni Conceicao aahidi ubingwa 2021