Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NGO’s), Vickness Mayao ameyaondoa Mashirika zaidi ya 158 kwenye Rejista ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Hayo yamesema jijini Mbeya na Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa NGO’s kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Grace Mbwilo kwa niaba ya Mkurugenzi na Msajili wa NGO’s nchini.
Amesema kuwa katika Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Namba 24 ya Mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa Mabadiliko na Sheria Namba 3 ya Mwaka 2019, imefafanua bayana kuwa jukumu la kusajili mashirika yanayoendesha shughuli za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, utawala bora, haki za kibinadamu na mazingira katika ngazi ya jamii kwa lengo la kutogawana faida na ambazo hazina mlengo wa kukuza biashara, zimeelekezwa kusajiliwa na Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s).
“Mashirika yaliyoondolewa kwenye daftari la Msajili wa NGO’s ni yale ambayo yalisajiliwa chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 ambayo yanafanya kazi kwa lengo la kunufaisha wanachama wake, kugawana faida, yenye mlengo wa dini yenye lengo la kukuza biashara na Bodi za wadhamini,”amesema Mbwilo
Aidha, amesema kuwa hatua ya kuyaondoa mashirika hay kwenye daftari la msajili wa NGO’s imefikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Marekebisho Na. 3 ya mwaka 2019 iliyoanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Julai 2019.
Kwa mujibu wa Sheria, Mashirika hayo yanatakiwa kwenda kujisajili chini ya Sheria husika ikiwemo Sheria ya Jumuiya za Kijamii (Sura ya 337), Sheria ya Munganisho wa Wadhamini (Sura ya 318) na Sheria ya Makampuni (Sura ya 212), na kwamba inatakiwa kukamilisha zoezi hilo kabla ya tarehe 01 Septemba,2019.
Katika kuhitimisha zoezi la usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali liliofanyika Mkoani Mbeya, Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali imewaagiza wadau wa mashirika yote yaliyosajiliwa kwa lengo la kuzalisha faida na kugawana faida kuhakikisha kuwa wanahamisha usajili ili kuhuisha taarifa zao kwa Msajili stahiki.