Eva Godwin – Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ameyataka Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini – NGO’s kulinda maadili na kuheshimu mila, desturi na tamaduni za Kitanzania wakati wa shughuli za utekelezaji wa programu zao mbalimbali.
Dkt. Mpango ametoa wito huo wakati akifunga Jukwaa la Tatu la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali – NGO’s lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijiniDodoma na kuwataka pia kuzingatia sheria za nchi na kufuata miongozo mbalimbali inayoratibu shughuli za mashirika hayo.
Amesema, NGO’s hizo zinatakiwa kuhakikisha hazitumiki kuharibu maadili ya Tanzania kwa kutekeleza ajenda binafsi zisizofaa. Ametoa wito kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii kufanya uchambuzi makini wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kuishauri Serikali juu mwenendo na ufanisi wa mashirika hayo.
Aidha, Dkt. Mpango pia amesema suala la mabadiliko ya tabianchi linapaswa kuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, kwani Tanzania ni miongoni mwa Mataifa yalizoathiriwa na hali ya hewa isiyotabirika.