Maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wamefanya ukaguzi wa kushtukiza katika masoko yaliyopo wilayani Musoma mjini Mara ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa shirika hilo kuondoa bidhaa ambazo hazina ubora kwenye soko nchini.
Ukaguzi huo umekwenda sambamba na kuondoa kwenye soko nguo za ndani za mitumba kutokana na matumizi yake kupigwa marufuku nchini kwa kuwa zina madhara kiafya kwa watumiaji.
Mbali na hatua hiyo, pia sampuli mbalimbali za bidhaa zimechukuliwa katika masoko hayo kwa lengo la kwenda kuzipimwa kwenye maabara za shirika hilo ili kujiridhisha kama zinakidhi viwango, huku vilainishi vya magari visivyokuwa na ubora vikiondolewa kwenye soko, kwenye baadhi ya maeneo ya kanda ya ziwa ambako operesheni hiyo imefanyika.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo Mkaguzi wa TBS, Baraka Bajije, amesema kuwa katika ukaguzi huo unaendelea Kanda ya Ziwa kabla ya Musoma Mjini umefanyika pia masoko maeneo ya Mwanza Mjini, Sengerema, Magu, Bunda na sasa Musoma Mjini ambapo wamefanikiwa kukamata shehena ya nguo za ndani za mitumba pamoja na taulo zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. milioni 10.
Amesema kuwa Sheria ya Viwango Namba 2 ya mwaka 2009 inazuia matumizi ya nguo za ndani za mitumba pamoja na taulo, lakini bado watu wasiowaaminifu wamekuwa wakiziingiza kwenye soko la Tanzania kupitia njia za panya.
Pia Bajije amesema bidhaa hizo haziruhusiwi kabisa kuwepo sokoni kutokana na madhara yake kwa watumiaji ikiwemo kusababisha magonjwa sugu ya fangasi, kansa ya ngozi na magonjwa mengine.