Manispaa ya Dodoma imepiga marufuku biashara ya uuzaji wa nguruwe na bidhaa zake kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe.
Taarifa hiyo imetolewa na Daktari wa mifugpo manispaa ya Dodoma, Dk. Innocent Kimweri kufuatia mamlaka aliyopewa ya kifungu namba 17 cha sheria ya magonjwa ya mifugo namba 17 ya mwaka 2003.
Hivyo kuanzia sasa ametangaza rasmi kuweka zuio la kufanya biashara ya nguruwe pamoja na mazao yake hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo.
”Hakuna mnyama yeyote wa jamii ya nguruwe, ngiri nguruwe, au nguruwe wa kufugwa atakayeruhusiwa kuingia au kutoka nje ya wilaya ya Dodoma pasipo ruhusa ya maandishi kutoka kwa daktari wa mifugo wa wilaya ya Dodoma mjini” amesema Dk. Kimweri.
Vilevile amepiga marufuku kuingiza au kutumika kwa bidhaa yeyote itokanayo na Nguruwe ikiwemo, Mbolea, mkojo, kinyesi na damu bidhaa hizo zitatumika kwa ruhusa ya maandishi toka kwa daktari.