Jioni ya leo Jumapili, majira ya 1:00 mashabiki wa soka watashuhudia moja kati ya Derby kubwa duniani, maarufu na yenye msisimko baina ya klabu mpya ya mshambuliaji Mbwana Samatta, Fenerbahce ambayo itakuwa ugenini dhidi ya Galatasaray.
Katika Derby hiyo ya Super League (SL) baina ya Galatasaray dhidi ya Fenerbahce itakuwa ya kwanza kwake kama atapata nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi ikiwa ni pamoja na kocha wake mpya, Erol Bulut.
Mara baada ya kutua Fenerbahce, Samatta hakuwa na muda wa kupoteza kabisa moja kwa moja alijiunga na timu na kuanza mazoezi ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na mechi hiyo kubwa na yenye mvuto wa kipekee kutokana na uhasama uliyopo baina ya Galatasaray na Fenerbahce.
Galatasaray ambao watakuwa nyumbani kwenye mchezo huo, wameibuka na ushindi kwenye michezo yao miwili iliyopita ya mwanzoni mwa msimu huku timu mpya ya Samatta, wakifanikiwa kushinda mechi moja na sare.
Katika wiki hii ya tatu ya Super League, klabu ya Fenerbahce haijatangaza kupata kwa majeraha mchezaji wake yoyote wakielekea kwenye mchezo huo utakaopigwa katika dimba la Türk Telekom ambao utasimamiwa na mwamuzi, Ali Palabıyık.
Ikumbukwe katika misimu mitano ya hivi karibuni Fenerbahce imeshinda mchezo mmoja na mmoja sare ya 0 – 0 mbele ya Galatasaray ambao wao wameibuka na ushindi kwenye michezo mitatu.
Historia pia inawabeba Fenerbahce ambapo katika jumla ya michezo 126 waliyocheza mbele ya Galatasaray kwenye Super League, wameibuka na ushindi mara 50 wakati Galatasaray wakishinda mara 34 huku wakitoka sare 42.