Manchester United na Ajax Amsterdam zimefanikiwa kutinga fainali ya michuano ya Europa League baada ya kuziondosha timu za Celta Vigo na Olympic Lyon kwenye michezo ya mkondo wa pili ya nusu fainali iliyocheza usiku wa kuamkia leo.
Manchester United ikiwa nyumbani Old Trafford imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Celta Vigo. Manchester United ilipata bao lake kupitia kwa Marouane Fellaini aliyefunga kwa kichwa kabla ya Facundo Roncaglia kuifungia Celta Vigo bao la kusawazisha.
Aidha katika mchezo huo ilishuhudiwa timu hizo zikimaliza pungufu baada ya nyota wao wawili Eric Bailly na Roncaglia kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Ovidiu Alin Hategan kwa mchezo usio wa kiungwana.
Manchester United imefuzu fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1. Ikumbukwe kuwa Manchester United ilishinda bao 1-0 kwenye mchezo Wa awali.
Katika mchezo mwingine Ajax Amsterdam imefuzu fainali licha ya kufungwa mabao 3-1 na Olympic Lyon kwa mabao ya Alexandre Lacazette aliyefunga mara mbili na Rachid Ghezzal. Bao la Ajax limefungwa na Kasper Dolberg.
Ikumbwe katika mchezo wa awali uliochezwa Jumatano iliyopita huko Amsterdam Arena, Ajax Amsterdam iliifunga Olympic Lyon mabao 4-1 hivyo inafuzu hatu ya fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-4.
Hatua ya fainali ya michuano ya Europa League itachezwa Stockholm, Sweden Jumatano Mei 24 mwaka huu ambapo timu itakayoshinda itapata zawadi ya kikombe pamoja na kufuzu moja kwa moja katika michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao.