Beki wa pembeni wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Nickson Kibabage, amesema anaamini kama wakishirikiana vizuri na wachezaji wenzake kikosini, wanaweza kuipa mafanikio makubwa timu hiyo ambayo msimu ujao itakuwa na kazi kubwa ya kutetea mataji yake na kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Akizungumza jijini Dar es salaam baada ya kupata nafasi katika kikosi cha Young African kilichocheza kipindi cha kwanza dhidi ya dhidi ya Kaizer Chiefs kwenye Kilele cha Siku ya Mwananchi Jumamosi (Julai 22), amesema mashabiki wa Young Africans wasubiri kuona ushindani mkubwa msimu ujao.
“Nitatumia uwezo wangu kuhakikisha msimu ujao ninashirikiana na wachezaji wenzangu kutetea mataji yetu yote,” amesema Kibabage, ambaye ni mchezaji mpya katika kikosi hicho.
Amesema anashukuru ushirikiano anaopewa na wachezaji wenzake kikosini tangu alipoungana nao mpaka sasa.
Akizungumzia mchezo wao huo, amesema ulikuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa na kudai utawasaidia kufanya vizuri katika mechi zilizopo mbele yao.
“Mchezo ulikuwa mzuri, kila mchezaji aliweza kuonesha kiwango chake, kwa upande wangu ninazidi kujifunza vitu vingi ambavyo vitanisaidia siku zijazo,” amesema.
Aidha, amesema malengo yake ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ili atimize malengo aliyojiwekea.