Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila amesema hakuna mabadiliko makubwa ya kiuchezaji atakayoanza nayo ndani ya kikosi hicho ingawa jambo kubwa atakaloanza nalo ni nidhamu kwa kila mmoja wao ili waweze kutimiza malengo kwa pamoja.

Katwila aliyejiunga na timu hiyo baada ya kuachana na Ihefu FC alitangazwa juzi Jumatatu (Oktoba 23) kukiongoza kikosi hicho baada ya mtangulizi wake, Habibu Kondo aliyeanza nayo tangu msimu huu umeanza kutimuliwa kutokana na matokeo mabaya katika Ligi Kuu Bara.

Katwila amesema ni fahari kwake kupewa nafasi hiyo huku akiomba ushirikiano kwa wachezaji na viongozi kwa lengo la kuitoa timu hiyo sehemu moja kwenda nyingine kutokana na changamoto ya matokeo bora inayowakabili.

“Hatuko sehemu nzuri hivyo tunahitaji kushikamana ili kutoka hapa tulipo, nidhamu ndiyo nguzo kubwa itakayotupeleka kule tunapopahitaji, hivyo kila mmoja wetu anapaswa kutambua tunahitaji kutoka hapa kwenda mbali zaidi ya tulipo.

Aidha aliongeza licha ya presha iliyopo ndani ya timu hiyo ya kutopata matokeo mazuri ila hilo kwake halihofii kwani yupo tayari kupambana na changamoto zilizopo mbele yake huku akiamini kikosi hicho kina wachezaji wazuri na wazoefu.

Kondo aliiongoza Mtibwa katika michezo mitano na alipoteza mitatu na kutoka sare miwili huku kwa upande wa Katwila mechi yake ya kwanza itakuwa ni kesho dhidi ya Geita Gold itakayopigwa kwenye Uwanja wa Manungu Complex, mkoani Morogoro.

Ricardo Ferreira atamba kuibanjua Young Africans
Rais Dkt. Samia, Hakainde kuondoa vikwazo vya Biashara