Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ameongoza katika matokeo ya awali ya kura zilizopigwa nchini humo katika uchaguzi mkuu, huku chama kikuu cha upinzani cha People’s Democratic Party (PDP) kikiyakataa matokeo hayo.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, Buhari ameshinda katika majimbo saba kati ya 36 hadi sasa, wakati mpinzani wake mkuu Atiku Abubakar akishinda majimbo manne ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Abuja.
PDP wamedai kuwa matokeo hayo yamechakachuliwa na hivyo hawayakubali kwani sio matokeo sahihi. Mwenyekiti wa chama hicho, Uche Secondus ameeleza kuwa Serikali pamoja na mawakala wengine wameonekana kuungana kuchakachua matokeo. Hata hivyo, hakueleza kwa vielelezo kuhusu madai hayo.
Umoja wa Ulaya, Marekani pamoja na Umoja wa Afrika wameeleza kuwa kulikuwa na mapungufu hususan ucheleweshwaji wa zoezi la upigaji kura hasa Jumamosi, lakini hakuna chombo chochote huru cha uangalizi ambacho kimedai kuwa kulikuwa na udanganyifu.
Rais Buhari anatafuta nafasi ya kuchaguliwa kwa muhula wa pili akipeperusha bendera ya chama cha All Progressives Congress (APC), kuliongoza taifa hilo lenye utajiri wa mafuta, lakini linalokabiliwa na changamoto ya umasikini kwa wananchi wengi, rushwa na ugaidi unaoongozwa na kundi la Boko Haram.
Matokeo mengine bado hayajatangazwa, na matokeo ya mwisho yatakayotangazwa na Tume ndiyo yanayosubiriwa kwa hamu.