Nigeria imemwita balozi wa Afrika Kusini nchini humo na kutuma ujumbe jijini Pretoria ili kuelezea masikitiko makubwa dhidi ya raia wake kushambuliwa, huku Umoja wa Afrika na Zambia nazo zimelaani vurugu hizo.
Rais Muhammadu Buhari amechukua hatua hiyo kufuatia magenge ya raia wa Afrika Kusini kuvamia biashara katika sehemu tofauti za nchi hiyo, wakipora mali na kuchoma magari katika wimbi jipya la chuki dhidi ya wageni.
Buhari alimuagiza waziri wake wa mambo ya nje kumuita balozi wa Afrika Kusini ili kuelezea masikitiko yake juu ya vitendo wanavyofanyiwa raia wa Nigeria na kutaka hakikisho la usalama wao pamoja na mali zao.
Aidha, Serikali ya Nigeria kupitia Ukurasa wake wa Twitter iliandika kwamba ujumbe wake utawasili jijini Pretoria siku ya Alhamis na kukutana na rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Rais Ramaphosa amelaani mashambulizi hayo akisema hayakubaliki.
Pia, msanii kutoka Nigeria, Tiwa Savage aliyekuwa ahudhurie hafla ya ‘DSTV Delicious Festival’ ametangaza kutoshiriki sambamba na msanii mwingine, Burna Boy kueleza kuwa hatokanyaga tena nchini humo hadi mambo yatakapotulia.
Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter Savage ameandika, “Sitokwenda kushiriki DSTV Delicious Festival jijini Johannesburg Septemba 21, 2019, maombi yangu kwa wahanga na familia zilizoguswa.”