Mabingwa watetezi wa ligi ya Ujerumani FC Bayern Munich, wataingia uwanjani mwishoni mwa juma hili kucheza dhidi ya wapinzani wao katika kilele cha msimamo wa Bundesliga RB Leipzig, bila ya kiungo wao Leon Goretzka.

Goretzka mwenye umri wa miaka 24, alipatwa na majeraha la paja la mguu wa kushoto akiwa katika mazoezi ya kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani juma lililopita, na tayari imeshaelezwa atafanyiwa upasuaji mdogo.

Meneja wa mabingwa hao wa Bundesliga Niko Kovac, amesema anatambua ugumu wa kukosekana kwa kiungo huyo, lakini atajitahidi kuziba pengo lake, ili kufanikisha mikakati ya ushindi ndani ya dakika 90 dhidi ya RB Leipzig.

“Goretzka alikua na umuhimu mkubwa kuelekea mchezo wetu wa mwishoni mwa juma hili, lakini sina budi kukubaliana na hali halisi, nitafanya kila linalowezekana ili kuziba kikamilifu pengo lake.” Amesema Kovac alipozungumza na waandishi wa habari.

FC Bayern Munich wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya Bundesliga, baada ya kilazimishwa sare ya mabao mawili kwa mawili dhidi ya Hertha Berlin majuma mawili yaliyopita.

Kwa matokeo hayo FC Bayern Munich walifikisha alama saba, huku RB Leipzig, wakijitanua kileleni kwa kumiliki alama tisa, zilizotokana na ushindi wa michezo mitatu iliyochezwa tangu kuanza kwa mshike mshike wa ligi ya Bundesliga msimu huu wa 2019/20.

Matokeo ya mchezo wa mahasimu hao utatoa picha kamili, kama RB Leipzig wataendelea kuongoza msimamo wa ligi, ama kuwapisha mabingwa watetezi kukaa kileleni.

TFF yashtakiwa FIFA.
Bilionea Jack Ma ajivua madaraka Alibaba