Meneja wa klabu bingwa nchini Ujerumani FC Bayern Munich Niko Kovac, amesema hafahamu lolote kuhusu mpango wa kuondoka kwa beki wake Jerome Boateng, ambaye anahusishwa na taarifa za kuwa mbioni kusajiliwa na klabu za PSG (Ufaransa) na Man Utd (England).
Kovac aliwaambai waandishi wa habari kutokua na taarifa za mchezaji huyo kuwania na klabu hizo, baada ya mchezo wa kirafiki ulioshuhudia kikosi chake kikiichapa Man Utd bao moja kwa sikuri usiku wa kuamkia leo, huku Boateng akiwa mmoja wa wachezaji waliofanikisha ushindi huo.
Meneja huyo kutoka Croatia amesema mpaka sasa hajapata taarifa zozote kuhusu beki huyo, na hadhani kama ataondoka katika kipindi hiki, kutokana na kuwa kwenye mipango yake ya msimu mpya wa ligi huko Ujerumani.
“Jerome amecheza soka safi sana leo (Jana) na alionyesha uwezo mkubwa wa kupambana wakati wote na kufikia hatua ya kuwazuia wapinzani (Man Utd).
“Ninafurahishwa na uwepo wake hapa, ninaamini ataendelea kuonyesha uwezo wake katika kipindi chote cha msimu mpya wa ligi ya Ujerumani, ambapo tutakua na kazi kubwa ya kutetea ubingwa wetu.”
“Kuhusu kuwa mbioni kuihama FC Bayern Munich, binafsi sifahamu lolote, kwani mpaka sasa sijapokea taarifa kutoka kwa viongozi wangu ambao wanapaswa kunieleza nini kinachoendelea kumuhusu mchezaji huyu”
“Sidhani kama ataondoka maana nimeshaweka wazi mipango ya kutaka kumtumia kwa msimu mpya wa ligi.” Alisema Kovac
Hata hivyo Boateng bado ana mkataba na FC Bayern Munich hadi mwaka 2021, na tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2011 akitokea kwa mabingwa wa soka nchini England Man City ameshatwaa mataji sita ya ligi ya Ujerumani (Bundesliga).
Fununu za kuondoka kwake klabuni hapo ziliibuliwa na mtendaji mkuu Karl-Heinz Rummenigge, ambaye aliwahi kukaririwa na vyombvo vya habari akisema huenda wakamuuza beki huyo mwenye umri wa miaka 29 kwenye klabu za PSG (Ufaransa) na Man Utd (England).