Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, amesema hatasau akikumbuka jinsi alivyovuliwa nafasi ya Uwaziri mwaka 2016 kwa madai kuwa alilewa, wakati siku ya tukio alikuwa anaumwa na alitumia dawa.
Kitwanga ameyasema hayo katika mahojiano maalum na Dar24 Media, na kudai kuwa mambo hayo hutokea katika siasa, kwani inawezekana kutengenezewa zengwe, kulongwa au kumalizwa kitu ambacho kilimfanya ahisi anatendewa jambo moja kati ya hayo.
“Wakati huo nilikuwa naumwa sana, nilikuwa nakunywa dawa, huwa sitaki sana kukizungumzia kitu hicho huwa kinaniumiza sana, kwa sababu nilijua, ninajua na wenyewe wanajua walichofanya, ila hayo yamepita kwa sababu ndio maana nasema tumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema Kitwanga.
Mwanasiasa huyo, alikuwa akinukuu maneno ya Balozi Humphrey Polepole ambaye awali pia alifanya mahojiano maalum na Dar24 Media na kuzungumzia mambo ya siasa, akiyataja mambo hayo matatu ya zengwe, kulogwa au kumalizwa.
Amesema, “huwa inaniumiza sana nikikumbuka jinsi nilivyovuliwa uwaziri, kwani nilijua, ninajua na wenyewe wanajua walichofanya, kwa Pombe gani ambayo inifanye niingie nimelewa, miaka mitano nilikua Naibu Waziri, na siku zingine nilikua najibu maswali ya wizara zaidi ya tatu, leo hii nikiwa ‘Full Minister’ ndio niingie nimelewa? Ni uzembe wa namna gani huo?.”
Hata hivyo Kitwanga amesisitiza kuwa, “Ni lazima utambue unaishi mara moja na dakika moja ikipita hairudi, kwa hivyo lazima ufurahie wakati uliopo,” huku akisisitiza kujituma katika kazi kwa uadilifu kwani MUNGU hufanya mengi katika siku za Binadamu awapo Duniani.”