Mfanyabiashara ya uuzaji wa Magari, Alex Muthee Mwangi ameshtakiwa Mhakamani kwa kumpiga na kumjeruhi Konstebo wa Polisi, Alphayo Baraza huku akisema alitenda hivyo ili kumfunza adabu.
Mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Milimani nchini Kenya, Lucas Onyina mtuhumiwa mbali na kukiri kumpiga Polisi huyo, alikana shitaka la kumjeruhi Konstebo huyo. Alphayo Baraza.
Mwangi alisema, ilibidi amtandike Afisa huyo wa polisi ili waheshimiane na kwamba ilimpasa ampe funzo kwani alimuudhi, huku akimuomba Hakimu wa Mahakama aliyemzuia kujitetea amuachilie kwa dhamana.
“Kama unataka kueleza hali ilivyokuwa utasema hayo kesi ikianza kusikilizwa. Tayarisha maelezo yako uyaseme siku ya kusikilizwa kwa kesi,” alisema Hakimu Lucas Onyina kumshauri mshtakiwa.
Awali, mbele ya Mahakama ilidaiwa na Kiongozi wa mashtaka, Anderson Gikunda kuwa, Mwangi ambaye anamiliki kampuni ya kuuza magari Mombasa na Nairobi, alimjeruhi Konstebo Baraza katika barabara ya Muindi Mbingu.
Alisema, Afisa huyo ambaye ni Trafiki alitofautiana na mshtakiwa Juni 27, 2023, kisha kupigwa huku Hakimu akikubali ombi la mtuhumiwa na kumuachiliwa kwa dhamana ya KSh 30,000 pesa taslimu hadi hapo Julai 13, 2023, kesi hiyo itakapotajwa tena.