Miaka ya 80-90, kuliibuka msemo wa ‘HAPENDWI MTU INAPENDWA POCHI,’ msemo huu ‘ulijimwambafai’ sana na kuchukua hatamu, kwani ulilenga faida zaidi kuliko utu na ulienda mbali zaidi kwani baadhi ya vitu muhimu hata vilivyohitaji usaidizi wa bure navyo vilipanda bei.

Nimeanza kwa kuongea hivi kwasababu thamani ya mtu ni utu sio vitu na ukipata nafasi ya kugusa maisha ya mtu fanya hivyo na Mungu atakubariki sana kwani huo ni mfano bora kabisa katika maisha ya hapa Duniani na ndivyo watu wanavyotakiwa kuishi.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na upungufu mkubwa wa watu wenye uthubutu, wenye kujiamini, wenye misimamo na ujasiri katika kusimamia uzalendo, haki na sheria za nchi miongoni mwa wabeba maono na watekelezaji wa sera wa nchi nyingi za Bara la Afrika.

Wengi kati ya waliobaki ni wale ambao unapokuwa katikati ya changamoto au mapambano watakwambia “endelea mbele tupo nyuma yako au tuko pamoja,” lakini usishangae utakapogeuka nyuma ukajikuta upo peke yako katika wakati ambao uliwahitaji kweli kweli.

Mara nyingi wengi kati ya watu wanaojinadi kuwa nyuma yako huwa ni wanafiki na wachumia tumbo wanaopima tu upepo wa kule unakoelekea na kukutanguliza kama chambo, na ukigeuka hutawaona na wala hawajui kuwa cheo au mamlaka ni koti la muda mfupi, muda wowote unaweza kulivua.

Hili ndilo jambo ambalo limepelekea wachambuzi na Wana-Pan-Africanism kutahadharisha kuwa bara la Afrika liko ukingoni mwa awamu mpya ya kinyang’anyiro cha rasilimali, ongezeko la matumizi ya silaha na kutawaliwa na mataifa makubwa ambayo yanaigeuza Afrika yatakavyo.

Mifano ipo mingi lakini mmoja wapo ni hatua ya kuandaliwa kwa mikutano ya kilele ya Kiafrika na mataifa ya kigeni katika nchi za Kiafrika jambo ambalo limezusha hali ya wasiwasi na kutoa mustakabali mbaya wa Bara zima la Afrika kwa Mataifa haya ya kigeni kuamua hatma ya Waafrika huku wakipigiwa makofi kwa shangwe.

Viongozi wa Afrika hawatangulizi ajenda ya umoja na kuweka kando harakati zao za kupata ruzuku ya bei nafuu ya chakula na kujali masilahi binafsi, kila mtu anangalia maslahi na kibaya zaidi ni maslahi binafsi, wanasahau kuwa wanapaswa kuungana na kuzungumza kwa sauti moja, ili kuja na hatma ya kulinda maslahi ya Waafrika wote.

Tumeona katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, nchi mbalimbali duniani zikiwemo Marekani, Urusi, India, China na Uingereza zimekuwa zikiandaa mikutano, makongamano ya kwao binafsi na hata ya kwetu huku Afrika, haya ni matukio ambayo kimsingi yanahusu majadiliano ya kiitikadi na kimkakati na viongozi wa Kiafrika la sivyo tunaangamia maana tusidhani tunapendwa sana hapana wanahitaji rasilimali zetu.

Hata hivyo, wachambuzi na Wana-Pan-Africanism wanaonya kuwa Afrika iko katika hatari ya kupoteza zaidi ya inachopata kupitia mashirikiano haya huku Wakosoaji wakisema Viongozi wa Kiafrika, hawana mamlaka ya kimaadili ya kuelekeza au kuongoza masuala ya kimataifa kinyume na matakwa ya mataifa ya nje.

Aidha, ongezeko la hivi majuzi la viongozi wa Afrika wanaozuru na kushirikiana na pande zinazozozana wakati wa mzozo wa Russia na Ukraine nao umezua hisia tofauti huku wachambuzi na Waafrika wakionya kwamba ushiriki huo unaweza bila kukusudia kuliweka bara hilo katikati ya mbio za matumizi ya silaha na migogoro baridi ya kivita.

Si mataifa makubwa yanayoitazama Afrika, hata nchi zinazokua kiuchumi kama Singapore na Mashariki ya Kati zimeonyesha nia ya kujongea kuja Afrika na hili linazua maswali kuhusu nini kinaifanya Afrika kuhitajika sana.

Licha ya wasiwasi huo, hakuna matumaini Afrika. Wachambuzi na Wana-Pan-Africanism wanasisitiza umuhimu wa viongozi wa bara hili kujitafakari na kuwa na maazimio ya pamoja kwani njia ya umoja pekee ndiyo itaiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili na kuhifadhi uhuru wake.

Nimalize kwa kunukuu mistari kadhaa ya Biblia kutoka katika kitabu cha Mithali 10: 7-14, humo kuna maneno yanasema, “Baraka humkalia mwenye haki kichwani; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.7 Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka; Bali jina la mtu mwovu litaoza.”

Mstari wa 8 unaendelea kusema, “Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.9 Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulikana.10 Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.”

Kisha mstari wa 11 unaendelea hivi, “Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,12 Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote.

Halafu 13 inasema, “Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu; Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.14 Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.”

Siongezi kitu ila niseme kwamba “NINGEJUA HUWA IPO NYUMA, WAKATI NI SASA VIONGOZI BARANI AFRIKA CHUKUENI HATUA.”

Adha ya Maji yapewa mkono wa kwaheri Momba
Rais amteua Binti yake kuwa mshauri wa Sera, Mikakati