Beki wa Young Africans ambaye kwa sasa yupo kwenye mzuka mkubwa Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amefunguka kuelekea mchezo wa Jumamosi (Mei 08), ambapo Simba SC watakua wenyeji wa Young Africans katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Ninja amefunguka kuhusu maandalizi ya mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, kufuatia upinzani wa timu hizo ambazo zina historia kubwa katika Soka la Bongo.

Ninja amesema mchezo huo utakua mgumu, kutokana na kila upande kuhitaji alama tatu muhimu, huku wao kama Young Africans wakihitaji zaidi alama hizo, kutokana na mazingira yaliopo kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa.

Beki huyo mzaliwa na visiwani Zanzibar amesema amejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo dhidi ya SImba na kama atapata nafasi ya kucheza, atahakikisha anatimiza majukumu yake ipasavyo ili kulinusuru lango la timu yao.

“Nipo tayari kucheza huo mchezo, kama kocha atanipa nafasi nitahakikisha nitatimiza jukumu lango la kulinda lango la Young Africans lisipate madhara kwa dakika zote 90.” Amesema Ninja.

Kuhusu kasi na umahiri wa mchezaji wa Simba SC Luis Miquissone, Ninja amesema: “Washambuliaji wote wa Simba nimewahi kukutana nao wala sina wasiwasi nao, kikubwa nawapa heshima tu kwa kuwa nao ni wazuri ila siwezi kuogopa lolote tukikutana wanajua hilo,” alisema Ninja.”

“Pale Simba mtu ambaye sijawahi kukutana naye ni Miquissone tu lakini naye tayari najua jinsi gani ya kuweza kukabiliana naye, ni mchezaji mzuri ila hutakiwi kumpa nafasi ya kufanya uamuzi anaweza kuleta madhara.”

“Hao wengine ni kwamba kila hatua unatakiwa kuanza kuamua wewe kabla ya wao hawajaamua na hilo hata kocha wetu (Nesreddine Nabi) amekuwa akitusisitizia kwamba ni makosa beki kuacha mshambuliaji afanye uamuzi kabla yako na hili sio gumu kwangu na naamini hata kwa wenzangu,”

Ninja alipata nafasi ya kucheza mchezo dhidi ya Simba SC kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mwezi Januari 2021, ambapo Young Africans waliibuka na ushindi kwa changamoto ya Penati.

Mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Novemba 2020, Ninja hakupata nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Young Africans, huku nafasi ya ulinzi wa kati ikizibwa na mabeki Lamine Moro na Bakari Nondo Mwamnyeto.

Simba SC inakwenda kucheza mchezo wa Jumamosi (Mei 08) ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufiksha alama 61, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 57 huku Azam FC wakishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 54.

ATCL yasitisha safari za India
Watu 23 wafariki baada ya flyover kuvunjika