Mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amesema yupo tayari kwa mazungumzo na hasimu wake, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo ambaye ni mkuu kikosi cha akiba – RSF, ili kumaliza vita ya kugombea madaraka.
Viongozi hao wa Makundi hayo ya kijeshi, wamekuwa wakipigana tangu mwezi April, 2023 katika makabiliano ambayo Umoja wa Mataifa umesema yamesababisha mauji ya watu zaidi ya 5,000.
Aidha, kufuatia mapigano hayo zaidi ya watu Milioni 5 waliripotiwa kuyakimbia makazi yao kutokana na vita hivyo, huku wengi wao wakiishi katika kambi za wakimbizi za nchi jirani na hivi karibuni pia Burhan alionya kwamba vita hivyo vinaweza kuzikumba nchi zilizopakana na Taifa lake.
Burhan amesisitiza kuwa atafanya mazungumzo na Dagalo, iwapo atakubali kuwalinda raia kwa mujibu wa makubaliano yalioafikiwa katika mazungumzo ya pande zote hivi karibuni jijini Jeddah nchini Saudi Arabia Mei, 2023.