Tume ya Taifa ya umwagiliaji – NiRC, imejipanga kuendelea na utekeleza wa miradi itakayoongeza eneo la umwagiliaji lenye ukubwa hekta 256,185.46, ili kufikia hekta milioni 1,200,000 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi – CCM ya 2020.
Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Julai 28, 2023 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Raymond Mndolwa amesema Ilani ya Chama ni muhimu itekelezwe, hivyo kufikia 2025 kila kitu kitakuwa kimefanyika kama inavyotakiwa.
“Maeneo ya kipaumbele katika Mwaka 2023/2024 ni katika Kukamilisha ujenzi wa skimu mpya 25 zilizoanza kutekelezwa katika Mwaka 2022/2023, kukamilisha ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu 30 zilizoanza kutekelezwa katika Mwaka 2022/2023,” amesema.
Hata hivyo, Mndolwa amesema Tume imepanga kutekeleza jumla ya miradi 822, ambapo miradi 114 ni ya ujenzi wa Mabwawa na 103 ni ya ujenzi na ukarabati wa Skimu za Umwagiliaji
Hata hivyo amesema wataanza kukamilisha ujenzi wa mabwawa 14 yenye mita za ujazo 131,535,000 yaliyoanza kujengwa Mwaka 2022/2023, kukamilisha usanifu wa mabonde 22 ya Umwagiliaji ulioanza Mwaka 2022/2023.