Kiungo wa klabu ya Young Africans na nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda (AMAVUBI) Haruna Fadhili Hakizimana Niyonzima, amenusurika kwenye ajali ya gari eneo Nyamata jijini Kigali.

Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa, Niyonzima alipata ajali hiyo alipokua akirejea jijini Kigali akitokea Wilayani  Bugesera.

Ajali hiyo ilitokea jana Novemba 18 wakati gari aina ya Fuso iliyokuwa ikijaribu kuipita baiskeli, ambayo ilikuwa mbele katika harakati hizo ndipo ikagonga gari ya Niyonzima aliyekuwa na rafiki zake watatu.

Niyonzima ambaye aliwahi kuitumikia Simba kwa miaka miwili kabla ya kurejea Young Africans mapema mwaka huu, amesema wametoka salama kwenye ajali hiyo na hakuna mtu aliyepata majeraha miongoni mwao.

“Niligongwa lakini jambo jema ni kwamba nipo salama, kilichoumia labda ni gari lakini hakuna hata mmoja ambaye aliumia kwenye ajali hiyo, niko salama,” aliongeza kiungo huyo fundi aliyewahi kupachikwa jina la mchezaji wa zamani wa klabu za Arsenal, FC Barcelona na Chelsea Francis Cesc Fabregas.

“Nilikuwa natoka kwenye mizunguko yangu ya kawaida, sasa wakati narejea nyumbani ndio yakatokea hayo,” amesema Nyonzima ambaye alirejea nyumbani kwao, baada ya kuitwa kwenye kikosi cha Rwanda kilichocheza dhidi ya timu ya taifa ya visiwa vya Cape Verde katika mchezao wa kuwania kufuzu fainai za Afrika (AFCON) 2022, lakini michezo yote miwili nyumbani na ugenini wakaambulia suluhu.

Kuhusu lini atarejea Tanzania kuendelea na majukumu yake ndani ya Young Africans, Niyonzima amesema kesho Ijumaa Novemba 20 atawasili Dar es salaam baada ya mambo yake ya kifamilia kukaa sawa. “Kuna mambo ambayo nilikuwa naweka sawa ya kifamilia ambayo kwa sasa yapo vizuri. Nitarudi kazi Ijumaa novemba 20.”

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 20, 2020
Simon Patrick aeleza kilichomuondoa Young Africans