Kocha Msaidizi wa Mbeya Kwanza FC Nizar Khalfan ametoa pongezi kwa wachezaji wake kwa kazi kubwa walioifanya kwenye mchezo wa jana Jumapili (Februari 06) dhidi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC.

Mbeya Kwanza FC inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara, ilikubali kichapo cha 1-0 licha ya kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi ya Simba SC kwa muda wote wa dakika 90.

Bao la ushindi la Simba SC lilipachikwa wavuni na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama dakika ya 80.

Nizar amesema wachezaji wake walionesha nidhamu kubwa kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na walifanikiwa kuidhibiti Simba SC iliyokua inalisakama lango lao kwa udi na uvumba, huku wao wakifanya mashambulizi ya kushtukiza.

“Wachezaji wangu wameonesha uwezo mkubwa sana, sina budi kuwapongeza kwa hilo, walipambana wakati wote na hii inaonyesha Mbeya Kwanza ina wachezaji wa aina gani hasa linapokuja suala la kufuata wanachoelekezwa.”

“Umeona namna walivyocheza na Simba walivyokua wanahaha kusaka bao, lakini bahati haikuwa kwetu tumepoteza mchezo huu, tunajipanga kwa mchezo mwingine.” Amesema Nizar Khalfan.

Kuhusu uhalali wa bao la Simba SC, Nizar amesema imewaumiza sana kwani kwa asilimia kubwa wanaamini halikua bao halali, kufuatia Meddie Kagere alikua eneo la kuotea kabla ya bao kufungwa.

“Inaumiza sana, watu wote wameonea mpira, kosa limeonekana hadharani, lakini yote kwa yote ndio soka, hatuna budi kukubaliana na matokeo na kuangalia namna ya kusonga mbele katika mapambano yetu.” Ameongeza Nizar.

Kwa ushindi wa bao 1-0 Simba SC inafikisha alama 31 zinazowaweka katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Mbeya Kwanza ikishika nafasi ya 12 ikiwa na alama 13.

Masau Bwire autilia mashaka ushindi wa Simba SC
Munalove:Msifanye upasuaji kuongeza shepu