Watoto wanne wa familia moja ya kijiji cha Machochwe mkoani Mara wamefariki dunia huku wawili wakinusurika kifo baada ya kula ugali wa muhogo unaodhaniwa kuwa na sumu.
Ofisa mtendaji wa kata ya Machochwe, Yohane Ole amesema watoto hao Joseph Michael (13), Zablon John (5), Neema Michael (4) na Neema John (3) walifariki Desemba 7.
Jana, Mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Machochwe, Joseph Kiberenge amesema kuwa watoto hao walikula ugali wa mihogo michanga ambayo haikuandaliwa vizuri, hali ambayo wanahisi ilitengeneza sumu.
” Kutokana na ukosefu wa chakula, walichimba mihogo michanga ya miezi mitano, bahati mbaya haikuvundikwa vizuri kisha wakasaga wakapikwa ugali. watoto walipata madhara kwakuwa kinga yao ni ndogo tofauti na watu wazima” alisema Dkt. Kiberenge.
Awali, watoto wawili waliofikishwa hospitalini hapo walikuwa wakilalamika maumivu makali ya tumbo, kutapika na kuishiwa nguvu.
Amesema kuwa Unga na baadhi ya sampuli zao zimepelekwa kwa mkemia mkuu Mwanza ili kujua ni sumu ya aina gani iliyo waua watoto hao.
Mama wa watoto hao, Maria Michael amesema walikuwa hawana uhakika wa kula, wakaamua kutengeneza unga wa mihogo hiyo michanga.
“Ukigeuka huku watoto wanalia hawajala kitu, ikanilazimu kusaga unga huo” ameeleza Maria huku akilia.
Ameeleza kuwa familia yao ina watu 14 na wanaishi kwa mlo mmoja pekee kwa siku na wakati mwingine kwa uji pekee, na siku hiyo alilazimika kusaga udaga kutokana na mihogo ya miezi mitano aliyokuwa amechimba.
Amesema baada ya kula siku hiyo, usiku wa manane watoto walianza kulalamika maumivu makali ya tumbo, aliwapeleka zahanati ya Marenga lakini wawili walifia njiani, waliporudi nyumbani wakakuta wawili wameshakufa pia huku wawili wakiwa hoi.
Ofisa kilimo wa kata ya Machochowe, James Hitler amesema hali ya chakula ndani ya kata hiyo ni mbaya, ukame na Tembo kuvamia mashamba ndiyo vinachangia hali hiyo.
Pia ameongeza kuwa hadi sasa eka 239 katika kijiji hicho zimeliwa na Tembo na wananchi hawajalipwa kifutia machozi, Debe la Mahindi limepanda kutoka Tsh, 7,500 hadi 19,500, Muhogo kutoka Tsh 5,000 hadi 10,500 katika kata hiyo.