Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amepokea lita 3,885 za viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu , vyenye thamani ya shilingi milioni 52 za kitanzania, kutoka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kupitia kiwanda chake cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) cha mkoani Pwani

Akizungumza mara baada ya kupokea viuadudu hivyo Malima amekishukuru kiwanda cha TBPL kwa kuwakopesha dawa hizo na kusema kuwa zitawasaidia kupambana na ugonjwa wa Malaria katika mkoa huo

”Tunataka ifike mahali tuseme tumepambana na kuua mbu kwa dawa iliyo tengenezwa na kiwanda kinacho simamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwani kinga ni bora kuliko tiba,” Amesema Malima.

Aidha amesisitiza kuwa lengo lao ni kuona mkoa wa Mara unakua mfano katika harakati za kupambana na Malaria duniani

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, Mkurugenzi wa Fedha wa NDC, Bi. Rhobi Sattima amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa utayari na uzalendo wake wa kununua viadudu hivyo, na kumpongeza kwa moyo wake wa kujali afya za wananchi wake kwa kuamua kuunga mkono juhudi za kutokomeza Malaria.

Dawa hizo za viuadudu zipo za aina mbili, ambavyo kuna vile vinavyo wekwa kwenye maji machafu (Gliselesf) na kwenye maji masafi (Bactivec) na havina madhara kwa binadamu na viumbe wengine kwani vinalenga kumuangamiza kiluwiluwi wa mbu pekee.

Kwasasa mahitaji ya dawa za viuadudu katika mkoa wa Mara ni lita elfu 20 na mkuu huyo wa mkoa ameahidi kuagiza dawa zaidi ili kufanya jitihada za kupambana na ugonjwa wa Malaria mkoani Mara kuwa endelevu.

Lema,Gambo wapigana vijembe
Wanne mbaroni, tuhuma za mauaji ya kiongozi UVCCM Iringa