Wakati Simba SC ikiongeza dozi ya mazoezi kwa wachezaji wake ili kujiandaa na mechi ya ufunguzi ya African Football League (AFL), dhidi ya Al Ahly kutoka Misri, watani zao Young Africans wanaendelea kujiimarisha kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC utakaochezwa Oktoba 25, mwaka huu.
Simba SC itawakaribisha A Ahly katika mechi hiyo ya ufunguzi itakayofanyika Oktoba 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu Wa Simba, Roberto Oliveira Robertinho’ amesema mbali na mazoezi ya uwanjani, ameanza kuwasoma wapinzani wao Al Ahly kwa kutizama picha za video za mechi walizocheza hivi karibuni kwa lengo la kufahamU ubora na madhaifu yao.
Robertinho amesema licha ya kikosi chake kutokamilika kutokana na baadhi kwenda kutumikia majukumU ya nchi zao, analazimika kuwapa mbinu nyota waliobakia huku watakapokamilika atafanya programu nyingine maalumu.
Amesema Al Ahly ni timu kubwa na yenye uzoefu wa kushiriki michuano mikubwa huku pia ikiwa na kikosi chenye wachezaji bora, hivyo wanajiimarisha ili kuwakabili kwa nguvu.
Kocha huyo amesema anaimani Simba SC pia ni wakubwa na wanaweza kupata matokeo mazuri katika mchezo huo na ule wa marudiano utakaochezwa Misri.
“Tumekuwa tukifanyia kazi mechi baada ya mechi, tulifanya vizuri mechi za ligi na sasa tunasuka kikosi chetu kuelekea mchezo dhidi ya Al Ahly, tunafahamu Ubora wa wapinzani wetu lakini pia wana madhaifu yao.
Ameongeza mipango yake ni kuona Simba inaendelea kupata matokeo mazuri ikiwamo kushinda mechi ya ugenini dhidi ya Al Ahly.
Wakati huo huo Simba leo watazindua rasmi wiki ya hamasa kuelekea katika mechi ya ufunguzi wa michuano ya AFL kwa kuandaa Simba Beach Bonanza litakalofanyika kwenye ufukwe wa Coco, jijini Dar es salaam.
Naye Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema anafanyia kazi makosa mbalimbali yaliyojitokeza katika mechi walizocheza ili kurejea katika ligi hiyo wakiwa imara zaidi.
“Tunahitaji kuwa imara zaidi, kila timu inajipanga kusaka ushindi, hakuna mechi rahisi, muda huu wa mapumziko ni wa kujimarisha katika kila idara,” Gamondi amesema kwa kifupi.