Mshambuliaji mpya wa Man City, Manuel Agudo Durán (Nolito) amesema alikataa ofa ya kujiunga na mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona, kwa ajili ya kutimiza lengo la kucheza soka lake chini ya utawala wa Pep Guardiola.

Nolito mwenye umri wa miaka 29, alionyesha uwezo mkubwa akiwa na klabu ya Celta Vigo katika mshike mshike wa ligi ya nchini Hispania msimu wa 2015/16 na kufikia hatua ya kuwa gumzo katika vyombo vya habari huku akihusishwa na taarifa za kutakiwa na klabu kadhaa za barani Ulaya.

Nolito amesema tayari FC Barcelona walikua wamejiandaa kwa kila kitu dhidi yake lakini aliona hakuna haja ya kuendelea kucheza soka nchini Hispania, hasa baada ya kusikia Pep Guardiola anahitaji kumsajili kwenye kikosi cha Man City.

Amesema, ni vigumu kwa mchezaji yoyote kukataa ofa ya klabu kubwa kama Barcelona kutokana na mafanikio waliyoyapata pamoja na mipango waliyonayo kwa misimu ijayo, lakini kwake ilikua rahisi kutokana na kuamini uwezo na falsafa za Pep ambaye aliwahi kupita Camp Nou.

Hata hivyo amekiri kuvutiwa na klabu ya Barcelona kwa namna wanavyocheza soka leo la ushindani na wakati mwingine alitamani kusajiliwa kwenye klabu hiyo, lakini bado akasisitiza Pep Guardiola alikwamisha ndoto hizo kutokana na kuwa shabiki wake mkubwa.

“Ukweli ni kwamba Barcelona ni klabu nzuri na niliipenda sana lakini linapojitokeza jina la Pep katika akili yangu, ninaona ni bora kuwa na mtu huyu kuliko klabu, hivyo naamini hapa nitacheza soka kwa amani na utulivu,” Alisema Nolito

“Napenda kuwa chini ya meneja bora, na kwangu ninaamini Pep ni mtu sahihi katika soka langu na ninaamini nitafanya vizuri nikiwa na klabu ya Man City ambayo itakua na mtazamo tofauti.” Aliongeza Nolito

Historia ya mshambuliaji huyo inaonyesha aliwahi kukitumikia kikosi cha pili cha Barcelona (Barcelona’s ‘B’), kabla ya kujiunga klabu ya Benfica ya nchini Ureno na kisha alirejea nchini Hispania mara aliposajiliwa na Celta Vigo mwaka 2013.

Hull City Yadhaminiwa Na Kampuni Ya Kenya
Video: Dhamira ya Rais Magufuli Kuhusu Serikali Kuhamia Dodoma