Msimu wa sikuu za Christmas na Mwaka Mpya ilikuwa na neema kwa wafanyabiashara wengi nchini lakini iliacha vilio vya utapeli kwa baadhi wa wafanyabiashara hususan maeneo ya pwani waliojikuta wametoa mali halali na kupewa fedha bandia.

Baadhi ya wamiliki wa Maduka na watoa huduma za simu pesa wilayani Kibaha mkoani Pwani wamepata hasara kubwa baada ya kusambaa kwa noti bandia za shilingi 10,000 katika eneo hilo katika msimu wa sikukuu hizo.

Eneo la Maili Moja na Kibaha ndio maeneo yanayodaiwa kuathirika zaidi na udanganyifu huo wa kutumia noti bandia.

Mmoja kati ya wafanyabiashara wa Bar, Lubul Lebulu aliwaambia waandishi wa habari kuwa alibaini kuwa alipoteza shilingi 120,000 wakati akifunga mahesabu yake ya sikukuu ya Christmas baada ya kubaini kuwa kuna noti bandia zilizokuwa zimechanganywa na fedha halali.

“Kuna mzunguko mkubwa wa noti bandia hapa katika eneo letu. Sio mimi pekee, wafanyabiashara wengi wamepata hasara kama hii. Watu wanapaswa kuwa makini zaidi kwa sababu suala hilo limeshabainika,” alisema Lubul.

Kamanda wa polisi mkoa wa Pwani, Boniveture Munishogi alisema kuwa jeshi hilo linamshikilia kijana mmoja kuhusiana na tuhuma za kujihusisha na udanganyifu wa kutumia noti bandia. Aliwataka wananchi wote kuhakikisha wanaripoti polisi haraka pale wanapoona noti bandia ili kulisaidia jeshi hilo kufuatilia na kuchukua hatua.

Mbunge wa Chadema na Wananchi Wapinga Mahakamani Zoezi la BomoaBomoa
CCM wamshukia Lowassa kuhusu wafanyabiashara na Kodi