Klabu ya Biashara United, inaendelea kujiimariasha kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAF’.
Biashara United imeendelea kudhihirisha hilo baada ya kumtambulisha Notokely John Masasi, aliyesaini mkataba wa miaka miwili akitokea klabu Ken Gold FC ya Chunya mkoani Mbeya.
Masasi ametambulishwa na Uongozi wa klabu hiyo, kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za Biashara United Mara, akiwa mchezaji wa tano kusajiliwa katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa 2021/22.
Tangu jana Biashara United imekua kazini kufanikisha usajili wa wachezaji watakaowatumikia kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Shirikisho ‘CAF’.
Wengine waliosajiliwa klabuni hapo kuelekea msimu mpya ni Kassim Mdoe kutoka kwa Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’, Aniseth Revocatus kutoka Mwadui FC, Toyo Odongo Matthew kutoka Zoo United ya Kenya pamoja na Atupele Green kutoka Geita Gold FC.