Novak Djokovic ametangaza kujienguwa katika michuano ya wazi Tenisi ya Canada kwenye viwanja vya Toronto Sobeys kwa wanaume iliyopangwa kuanza kurindima Agosti 03 hadi 13.
Djokovic alitarajiwa kushiriki mcihuano hiyo kwa wanaume, na alisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wake nchini Canada, kufuatia umahiri wake wa kutwaa mataji makubwa 23 ya Grand slam.
Staa huyo kutoka nchini Serbia amejiondoa kwa ombi maalum kwa waandaji wa michuano hiyo, Chama cha Tenisi nchini Canada, akijipa muda zaidi wa kutulia kwa kinachoonekana kuvurugwa na kichapo kutoka kwa Carlos Alcaraz kwenye fainali ya Wimbledon.
Mkurugenzi wa michuano hiyo Karl Hale, amekiri kuvurugwa mno na kujitoa kwa Djokovic ambaye ameshinda michuano hiyo mara nne, pamoja na mashabiki pia waliotamani kumuona lakini akasisitiza bado kutakuwa na wachezaji wazuri watakaoshiriki.
Djokovic anapumzika akiwa na malengo ya kushiriki michuano ijayo ya tenisi Marekani (US Open) ambayo alishindwa kushiriki misimu iliyopita kutokana na ishu za Uviko-19 na hakuruhusiwa kuingia bila kuchanja kinga ya virusi hivyo.