Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC, Saido Ntibanzokiza ametoa onyo kwa mastaa wenzake ndani ya timu hiyo kwa kuwaambia kuwa kitendo cha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika wasione kuwa wamemaliza kila kitu kwa kuwa bado wana kazi nzito ikiwemo mchezo wa ufunguzi wa Michuano ya Africans Football League dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Ntibanzokiza ametoa kauli hiyo kufuatia Simba SC kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuwaondoa MAbingwa wa soka nchini Zambia Power Dynamo kwa faida ya bao la ugenini.
Saido amesema kuwa wana kazi kubwa ya kufikia malengo waliojiwekea msimu huu 2023/24, katika Ligi ya Mabingwa Barani Afika pamoja na michuano mipya ya African Football League Ligi inayotarajia kuanza Oktoba 20.
Nataka niwaambie wenzangu, kazi yetu kubwa ipo mbele yetu kwa sababu ya uzoefu wetu wa kucheza katika hatua hii ya makundi, lakini bado tunapaswa kujipanga kuhakikisha tunafanikiwa kufanya vizuri ili kufikia malengo pamoja na mashindano ya African Football League ambayo tunapaswa kufanya makubwa,” amesema Nibanzokiza.
Simba SC itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 20 kwa kuikaribisha Al Ahly katika mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Robo Fainali ya African Football League, kisha mchezo wa Mkondo wa Pili utachezwa juma moja baadae mjini Cairo.