Uongozi wa Simba umekaa kikao na kuazimia kuwaita mezani baadhi ya wachezaji wake wakiongozwa na washambuliaji Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ na Aubin Kramo ili kujadili mikataba yao.

Simba inataka kumwongezea Saido mkataba kabla haijafika Desemba ili kumzuia kuondoka kikosini hapo kwani mkataba wake wa awali (wa mwaka mmoja), aliousaini kwenye dirisha dogo la msimu uliopita akitokea Geita Gold utamalizika Desemba 2023.

Imefahamika kuwa tayari Saido na Simba SC wameanza mazungumzo kuhusu mkataba mpya na kila pande umewasilisha matakwa yake na mchakato wa majadiliano unaendelea vizuri.

Wakati Saido akiwa mbioni kusaini mkataba mpya, hali iko tofauti kwa Kramo, ambaye mabosi wa Simba SC wanapiga hesabu za kuachana naye kwenye dilisha dogo, Januari 2024 kutokana na kuandamwa na majeraha yanayomweka nje kwa muda mrefu.

Tangu alipojiunga na Wekundu wa Msimbazi, mwanzoni mwa msimu huu akitokea Asec Mimosas ya nchini kwao Ivory Coast, kiungo huyo mshambuliaji hajacheza katika mechi yoyote ya kimashindano.

Kramo yuko nchini kwao alikokwenda kwa matibabu, lakini imeelezwa viongozi wa Simba SC wapo tayari kufungua mazungumzo ya kuvunja mkataba ili kupata nafasi ya kusajili mchezaji mwingine na imepanga kushusha beki wa kimataifa.

Siasa zibadilishe maisha ya Watanzania - Dkt. Biteko
Ndyamkama ataka ubora wa kazi, usimamizi mikataba ya TARURA