Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ‘TPLB’ imebadili baadhi ya vipengele vya kanuni ya mfungaji bora endapo ikitokea wachezaji wawili wamefungana katika kinyang’anyiro hicho mwisho wa msimu kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto amesema kama wachezaji watafungana kwa mabao ya kufunga wataangalia ambaye hajafunga mabao au kufunga mabao machache ya Penati ndio atakuwa mfungaji bora.

Msimu uliopita, Fiston Mayele aliyekuwa Young Africans na Saido Ntibazonkiza wa Simba SC walifungana kileleni kwa mabao 17 na kila mmoja kupewa tuzo ya ufungaji bora kwa sababu kanuni hazikuwa zinasema chochote kuhusu hali hiyo.

“Tulipotunga hizi kanuni haya hatukuyaangalia sana, lakini kutokana na uzoefu wa msimu uliopita, tumejifunza na tumeweka wazi kanuni juu ya ufungaji bora, takribani majuma mawili yaliyopita tulikuwa na wenyeviti wa klabu na kanuni hii ilizungumzwa.

“Mfungaji bora ni yule mwenye mabao mengi, lakini kufungana inatokea, inapotokea ndio tunaangalia vigezo kwamba ukifunga bao la kawaida la dakika 90 lile linachukua pointi mbili na ukifunga kwa Penati ni pointi moja kwa hiyo hii itatusaidia kutofautisha mfungaji bora tunampata kwa jinsi gani,” amesema Mguto.

Aidha, mwenyekiti huyo alieleza kuwa muda si mrefu kanuni hizo zitawekwa wazi kwa umma na kufahamu mabadiliko mengine kama namna ya kumtafuta mchezaji bora wa ligi ikihusisha kigezo cha dakika alizoitumikia timu yake msimu mzima.



Antoine Griezmann kumfuata Messi Marekani
Wanahabari wajengewa uwezo matumizi ya Gesi mbadala