Mshambuliaji mpya wa klabu ya Young Africans Saido Ntibazonkiza amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, kuwa na subra katika kipindi hiki ambacho wanaendelea kuhangaikia ubingwa wa Tanzania Bara.
Ntibazonkiza ambaye alicheza mchezo wake wa kwanza Jumamosi dhidi ya Dodoma Jiji FC na kufunga bao miongoni mwa mabao matatu yaliyoipa ushindi Young Africans, amesema mashabiki na wanachama wanapaswa kuendelea kuiombea timu yao ili kufanikisha lengo la kutwaa ubingwa, ambao kwa msimu mitatu mfululizo umechukuliwa na Simba SC.
“Mashabiki na wanachama wanapaswa kuwa na subra, watuombee tuendelea kupambana vizuri na kupata ushindi katika kila mchezo, ninaamini tutafanikiwa In Shaa Allah.”
“Wakati nakuja hapa sikufahamu kiundani nitakutana na watu wa aina gani, nimehamasika sana baada ya kukuta kila mtu ndani ya Young Africans analia na ubingwa, ndiyo maana katika kila mchezo wachezaji hujitolea hadi mwisho.”
“Hilo limenifanya hata mimi sasa kutamani kuipa Young Africans ubingwa, Mungu akipenda msimu huu tutakuwa mabingwa.” Amesema mshambuliaji huyo.
Kesho Young Africans itacheza mchezo wa mzunguuko wa 17 wa Ligi Kuu Tanzania Bara jijini Mbeya dhidi ya Ihefu FC, Uwanja wa Sokione saa kumi jioni.
Young Africans ipo kieleleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 40 baada ya mechi 16, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 32 zilizotokana na michezo 14, wakati Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwa alama 29 kutokana na kushuka dimbani mara 16.