Baada ya Uongozi wa Young Africans kuthibitisha kumalizana na Kiungo Mshambuliaji Said Ntibazonkiza, imeelezwa kuwa Staa huyo kutoka nchini Burundi huenda akaonekana tena katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao 2022/23.
Saido ambaye aliingia matatani kwa madai ya utovu wa nidhamu wakati timu ya Young Africans ikijiandaa na mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Simba SC, anatajwa kuwaniwa na klabu ya Singida Big Stars (DTB FC) iliyopanda Daraja, kutoka Ligi Daraja la Kwanza.
Kiungo huyo anatajwa kuwa kwenye mazungumzo na Uongozi wa klabu hiyo, na huenda akasaini mkataba wa miaka miwili, ili kuendelea kuuwasha moto katika Ligi Kuu, baada ya kufanya hivyo akiwa Young Africans tangu Januari 2021.
Kwa sasa Saido yupo nchini kwao Burundi katika maandalizi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, inayojiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2023 dhidi ya Namibia Juni 04, kisha timu hiyo itacheza dhidi ya Cameroon Juni 08.
Wachezaji wengine wanaotajwa kuwa mbioni kujiunga na klabu ya Singida Big Stars ni Kiungo Mshambuliaji Deus Kaseke na Beki wa Kulia Paul Godfrey ‘Boxer’ ambao wote watamaliza mikataba yao na Young Africans mwishoni mwa msimu huu.