Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazonkiza amedai kushawishiwa na mawakala wa mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC, ili aachane na Young Africans na kujiunga na klabu hiyo ya Msimbazi.

Ntibazokinza alithibitishwa kujiunga na Young Africans siku moja baada ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Tanzania na Burundi uliochezwa mwezi uliopita jijini Dar es salaam.

Amesema mawakala hao walimfuata nchini kwao Burundi akiwa kwenye majukumu ya timu yake ya taifa na kumrubuni, lakini alionyesha msimamo wa kuheshimu taratibu za awali alizoafikiana na uongozi wa Young Africans.

“Nilifuatwa na watu wa Simba wakitaka nijiunge nao, nakuwa niwaeleze nalipwa kiasi gani, wao watanilipa vizuri zaidi”

“Sikuwa tayari kukubaliana nao kwa kuwa tayari nimeshasajiliwa na Young Africans na hata kiasi cha malipo ninayolipwa na Young Africans ni siri yangu na klabu. Nilitoa taarifa kwa uongozi juu ya watu hawa wanaonisumbua,” amesema Ntibazonkiza

“Binafsi sitaki kuumiza mioyo ya mashabiki wa Young Africans, wamenipokea vizuri na mimi niko tayari kuwatumikia”

Ntibazonkiza alisajiliwa na Young Africans ikiwa ni pendekezo la kocha Cedric Kaze, huku ikielezwa alipaswa kujiunga na klabu hiyo mapema zaidi kabla ya kuanza msimu huu 2020/21.

Anatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanza majukumu yake ndani ya kikosi cha Young Africans, na ataanza rasmi kuitumikia klabu hiyo Disemba 15 dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa.

Serikali yawapongeza Diamond, Nandy na Zuchu
Afrika Kusini yatoa hati ya kukamatwa kwa Mchungaji tajiri zaidi Afrika