Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC, Saido Nibazonkiza amesema matokeo waliyoyapata dhidi ya Al Ahly ya Misri sio mazuri sana na sasa wanajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mechi ya marudiano.
Wekundu hao walipata sare ya mabao 2-2 Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es salaam Ijumaa (Oktoba 20) ikiwa ni mchezo wa ufunguzi wa michuano mipya ya Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) inayoshirikisha timu nane.
Saido aliyetoa pasi ya bao la pili la Simba SC amesema wana furaha kwa matokeo hayo lakini sio waliyokuwa wakiyataka kwani ushindi ndio muhimu zaidi japokuwa anawapongeza wachezaji wenzake kwa namna walivyojitoa katika mhezo huo.
“Al Ahly ni timu kubwa na tunashukuru Mungu kwa matokeo haya, huu ni mchezo wa kwanza na sasa tunasubiri wa pili kuona tutafanya nini lakini binafsi nampongeza kila mchezaj, kila mmoja alipambana, hii ni sare ya 2-2 lakini kwenye mpira lolote linatokea, tusubiri mechi ya pili” amesema Saido.
Amesema kwa sasa wanakubaliana na matokeo hayo lakini wanakwenda kujipanga zaidi wakitambua mchezo wa ugenini hautakuwa mwepesi, akiamini kocha wao Roberto Oliveira Robertinho’ atakuwa na mbinu za kuwavuruga wapinzani wao nyumbani kwao.
Timu hizo zinatarajia kurudiana kesho Jumanne (Oktoba 24) kwenye Uwanja wa Cairo uliopo mjini Cairo huku Simba ikihitajį ushindi au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.