Tambo dhidi ya Simba SC zimeendelea kuchukua nafasi kinywani mwa Afisa Uhamasishaji wa Young Africans Antonio Nugaz, baada ya kikosi chao kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri, kwenye mchezo wa Machi 08 mwaka huu, Uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Nugaz ambaye aliongoza hamasa dhidi mashabiki na wanachama wa Young Africans kabla ya mchezo huo wa mkondo wa pili wa ligi kuu, amesema hawana hofu kabisa na watani zao Simba SC, na wako tayari kukutana nao tena kwenye michuano ya kombe kombe la shiiriksho (ASFC), ambayo droo ya hatua ya robo fainali ilitarajiwa kufanywa Jumatano ya juma hili, lakini iliahirishwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona.
Nugaz amesema wanaweza wasiwe na mwenendo mzuri sasa lakini haimaanishi kuwa wakikutana na Simba watafungwa “Hawa tukutane nao hata mara 10 msimu huu, bila ya makandokando hawatufungi ng’o!,” alitamba Nugaz
“Tena itakuwa vyema tukutane nao kwenye kombe la FA tuwaonyeshe kwa nini sisi tunabaki kuwa mabingwa wa kihistoria Tanzania”
Pamoja na mabadiliko makubwa ya kikosi chake, msimu huu Young Africans imezima tambo za watani zao Simba baada ya kuondoka na alama nne kati ya sita dhidi yao kwenye ligi, kutokana na matokeo ya sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa mkondo wa pili uliopigwa Mach 08.
Upo uwezekano miamba hiyo ya soka nchini ikakutana kombe la shirikisho la (ASFC) kama wote wataweza kutinga fainali au droo ikawakutanisha mapema.
Timu nyingine zilizotinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la shirikisho (ASFC) ni Azam FC, Kagera Sugar, Ndanda FC, Alliance FC, Namungo FC na Sahare All Stars ya ligi daraja la kwanza.