Afisa Mhamasishaji wa Young Africans Antonio Nugaz amesema klabu yao itakuja na taarifa rasmi kuhusu kinachoelezwa kuwa wamefungiwa kusajili kwenye madirisha matatu baada ya kushindwa kulipa kwa wakati fedha wanazodaiwa na mchezaji wao wa zamani Amisi Tambwe.
Mapema hii leo taarifa zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaeleza kuwa Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ ambalo liliagiza mshambuliaji huyo kuliopwa stahiki zake, limefikia maamuzi hayo baada ya kuona muda walioipa Young Africans kulipa deni kupita.
Nugaz amesema suala la kufungiwa kusajili wanaliona kwenye mitandao ya kijamii, na hawajapata taarifa rasmi kutoka FIFA, hivyo wamewataka mashabiki na wanachama wa Young Africans kusubiri tamko maalum kutoka kwa viongozi wao.
Hata hivyo amesema kaimu katibu mkuu wa young Africans Haji Mfikirwa alilizungumza jana wakati wa hafla ya Media Day Tour iliyofanyika Avic Town jijini Dar es salaam.
“Kuhusiana na suala la Amis Tambwe, tunaona kwenye mitandao na kusikia lakini jana kaimu katibu mkuu alilizungumza. Kama lipo kwa uhalisia huo, naamini litafanyiwa kazi na ofisi ya kaimu katibu mkuu Haji Mfikirwa ili kuweka kilakitu sawa.”
“Nimemuuliza Kaimu Katibu Mkuu kwa hiyo vyovyote itakavyokuwa tutakuja na taarifa rasmi lakini mpaka sasa hilo jambo lipo kwenye mitandao.”
Habari za uhakika kabisa kutoka Zurich nchini Uswisi zinaeleza kuwa Young Africans ilipewa siku 45 kumlipa mshambuliaji wake wa zamani Amissi Tambwe fedha anazodai ambazo alipaswa kulipwa tangu akiwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Young Africans bado hawajalipa hata senti kwa Tambwe ambaye anadai dola 19,000 ambazo ni zaidi ya Shilingi milioni 43.7 na FIFA imeitaka klabu hiyo kuongeza asilimia 5, ikiwa kama ya usumbufu kwa mchezaji huyo.
Tambwe anadai Young Africans fedha hizo ikiwa za mishahara ya miezi miwili pamoja na kiasi kidogo ambacho hawakumlipa katika fedha yake ya usajili.