Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa amefanya mahojiano na Kituo cha Luninga cha Clouds na kusema mkataba baina ya Serikali na Dubai wa ushirikiano wa uendelezaji wa Bandari, hauna tatizo na umeangalia maeneo yote muhimu na endapo ungekuwa na mapungufu angeingia Bungeni kuupinga.
Katika mahojiano hayo, Silaa ametumia muda mwingi kuutetea Mkataba huo na ‘kuwaponda’ wale wote wanaoukosoa akisema hawajausoma vizuri na wengine wanapotosha, na zifuatazo ni baadhi ya nukuu alizozitoa wakati wa mahojiano hayo.
1. “Mbowe amezungumzia Bandari katika mkutano wao Temeke lakini hakusema ni ibara gani zimesema juu ya hizo idadi alizosema kuwa zote zinafungwa na Mkataba wa uwekezaji jambo linaloendeleza upotoshaji huu.”
2. “Jambo hili kisheria halina tatizo lolote, ila huko nje kuna mtu anaweza kuamua tu kusema bila kufuata sheria na utaratibu ili azue taharuki. Hataki kujua umuhimu wa kusikiliza wengine kiasi cha kuingilia mamlaka ya habari.” Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa.
3. “Wanaosema bandari inauzwa, waonyeshe watu mahali panaposema mauziano, kwa sababu hata ibara ya 12 (1) inaongelea mambo ya ulinzi katika mkataba huu wa uwekezaji wa bandari na wala sio kuuziana kama watu wanavyojaribu kusema.” – Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa.
4. “Kwenye jambo hili wako wanaopotosha, kwa mfano ukimsikiliza Prof. Tibaijuka anachukua maana (definition) ya territory ilivyokuwa “defined” anasema nchi imetoa kila kitu, ardhi, anga na maji ambayo hasemi ni ibara gani imetamka maneno hayo.” Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa.
5. “Nimeanza kusema kwa sababu kuna watu wanapotosha umma. Jambo hili halina tatizo, ila huko nje kuna watu hawataki kuelewa umuhimu wa kufafanua jambo.” Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa.