Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani jana alitangaza kujiengua kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais wa shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na TFF, Nyamlani aliwasilisha barua kwenye shirikisho hilo jana Jumapili, siku moja tu tangu Kamati ya Uchaguzi ipitishe jina lake kuwa miongoni mwa wagombea 10 wanaowania nafasi hiyo ya urais.
Hata hivyo, hakukuwa na maelezo ya kina ya kujitoa katika kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu ikielezwa kuwa ni sababu binafsi.
Kutokana na uamuzi huo, hivi sasa wagombea tisa pekee ikiwa ni pamoja na Rais wa sasa, Jamal Malinzi anayetetea nafasi hiyo ndio watakaofanyiwa usaili June 29 mwaka huu.
Mbali ya Malinzi wengine wanaowania nafasi hiyo ni Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe.
Waliojitokeza kuwania Makamu wa Rais na kurejesha fomu wako Mulamu Ng’hambi, Michael Wambura, Geofrey Nyange, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.