Maafisa wa Shirikisho la Soka la duniani FIFA wanadaiwa kuchukua rushwa ili kuzipigia kura Urusi na Qatar kuwa wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022.
Taarifa hizo zimefichuliwa na waendesha mashtaka wa Marekani baada ya uchunguzi wa muda mrefu uliokuwa ukifanywa sFBI juu ya vitendo vya rushwa michezoni.
Nyaraka zilizotolewa na FBI zimeeleza kuwa waliokuwa maafisa kadhaa wa FIFA wakati huo “ama waliahidiwa au walipokea hongo iliyokuwa ikihusiana na mchakato huo wa upigaji kura”.
Maafisa wanaotajwa katika taarifa hiyo ni aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Amerika Kusini (CONMEBOL) Nicolas Leoz ambaye alifariki Agosti 28 mwaka jana na Ricardo Teixeira kutoka Shirikisho la Soka nchini Brazil.
Wengine ni Rafael Salguero wa Guatemala, pamoja na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Rais wa FIFA, Jack Warner kutoka Trinidad & Tobago anayedaiwa kupokea paundi milioni 4 (Tsh. Bilioni 11.4) ili kuipigia kura Urusi.