Makongoro Nyerere, mtoto wa baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere amempa ujumbe Rais John Magufuli, juu ya wanaobeza kazi iliyofanywa na serikali yake.
Akizungumza jana mjini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Makao Makuu ya Benki ya NMB, Nyerere alitumia maneno ya mwanafalsafa aliyeishi kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, akieleza kuwa hakuna mtu atakayependwa na kila mtu, na kwamba wapo ambao hawaridhiki hata wapewe nini.
Amesema kuwa kwa kipindi kifupi, anayafahamu mambo mengi mazuri aliyoyafanya Rais Magufuli ambayo kwa kuyaelezea tu yanahitaji kipindi maalum.
“Huwezi kupendwa na kila mtu. Ukiona unapendwa na kila mtu ujue kuna tatizo. Na ukiona unachukiwa na kila mtu pia ujue kuna tatizo,” alimnukuu mwanafalsafa huyo.
Aidha, Mbunge huyo wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki alisema kuwa moja kati ya mambo ambayo Mwalimu Nyerere aliyapa kipaumbele ni elimu kwa ajili ya wote, isiyofuata misingi ya matabaka.
Alisema mtazamo huo ndio uliosababisha Mwalimu Nyerere kuzitaifisha shule zilizokuwa zinamilikiwa na Kanisa Katoliki ambazo moja kati ya vigezo vya kudahiliwa ilikuwa ni kuwa Mkristo.
Nyerere alisema kuwa taifa linahitaji kuipa elimu kipaumbele kama ifanyavyo Serikali ya Rais Magufuli. Alisema Serikali ya kikoloni ilikuwa na lengo la kutoa elimu kwa watu wachache ikihofia kupata watu wengi wenye upeo zaidi ambao wangeweza kuanza kudai uhuru kama alivyofanya Mwalimu Nyerere na viongozi wengine.