Katika kuenzi kazi na kuthamini kazi walizofanya waasisi Mwl. Julius Nyerere na Oliver Tambo, picha za viongozi hao walioacha alama ulimwenguni, zimechorwa katika Ofisi ya Ukombozi wa Afrika, ili kuweka sawa kumbukumbu ya historia ya ukombozi wa Afrika Kusini.
Hayo, yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu Novemba 25, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa picha maalumu zinazoonesha wapigania uhuru wa mwanzo wa Afrika Kusini waliofika Tanzania kuandaa harakati za ukombozi wa nchi yao.
Amesema, katika kutekeleza azma hiyo, Serikali ya Tanzania imefanya ukarabati jengo la yaliyokuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambapo mipango na mikakati yote ya Umoja wa Afrika ya kuzikomboa nchi za Afrika ilifanyika ambalo linatarajiwa kufunguliwa Desemba 2022 ikiwa ni Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika.
Yakubu ameongeza kuwa, watanzania wanajivunia ushirikiano kati yao na Afrika Kusini na urithi huo ambao umechorwa kwenye kuta za jingo hilo ni ukumbusho unaodhihirisha kuwa nchi hizo ni zaidi ya kaka na dada na hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wake wanaishi kulingana na maono ya waasisi wake.
Awali, Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni kutoka Afrika Kusini Nocawe Mafu amewashukuru Mzee Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Oliver Reginald Tambo na kusema wachoraji Teboho Elisha Motigoe kutoka Afrika Kusini na Lutengano Mwakipesile kutoka Tanzania wamechora picha ambazo zinawakilisha mambo yaliyofanyika na kupepelekea kuptikana uhuru wa Afrika Kusini.
Amesema, “Hatuwezi kuzungumzia uhuru wa Afrika Kusini bila kuzungumzia kazi iliyofanywa na Tanzania, nachukua fursa hii kuwashukuru Watanzania kwa mchango wao kwetu, tunazungumza leo Afrika ya Kusini ipo huru, Nyerere aliruhusu harakati za ukombozi kutoka Afrika Kusini kufanyika Tanzania na kujenga nyumba zao hapa.”