Nyoka wawili weusi wamekutwa ndani ya ofisi ya Rais wa Liberia, George Weah hali iliyomlazimu kuhama ofisi yake kwa muda.
Mkurugenzi wa Masuala ya Habari wa Ikulu, Smith Toby amekaririwa na BBC akieleza kuwa nyoka hao wawili walikutwa Jumatano katika ofisi za mkuu huyo wa nchi ambazo ziko kwenye jengo la Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje.
Kutokana na hali hiyo, wafanyakazi wote waliokuwa wanatumia jengo hilo wametakiwa kutoenda tena kazini hadi Aprili 22, kupisha shughuli za kuwaondoa nyoka hao pamoja na wadudu/wanyama wengine wasiohitajika.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa wanyama na wadudu wote wanaotambaa au wanaoruka wanaondolewa kwa kupuliza dawa za kuua wadudu (fumigation),” alisema Tody.
“Wizara ya Mambo ya Nje ndiyo yenye ofisi za Rais, kwahiyo imetoa tangazo la ndani kwa wafanyakazi wake kubaki nyumbani wakati ambapo kazi ya kupuliza dawa maalum za kuwaondoa wadudu na wanyama ikiendelea,” aliongeza.
Tody alisema kuwa nyoka hao wawili walioonekana hawakuuawa, walifanikiwa kupata upenyo kwenye tundu moja na kutokomea kusikojulikana.
Ofisi ya Rais imekuwa ndani ya jengo la Wizara ya Mambo ya Nje tangu mwaka 2006 baada ya moto mkubwa kuteketeza moja kati majumba ya makazi ya Rais.
Polisi na kikosi maalum cha ulinzi wa Rais walionekana wakiwa wameongeza ulinzi kwenye eneo la makazi ya Rais katika Mji Mkuu wa Monrovia.