Saa 24 baada ya kuachana na Simba SC, Mchezaji Kiraka Erasto Edward Nyoni ametambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa Namungo FC, hivyo ataendelea kuonekana katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Nyoni alieitumikia Simba SC tangu mwaka 2017, ameondoka klabuni hapo akiacha kumbukumbu ya kuwa sehemu ya kikosi kilichofika Robo Fainali Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika zaidi ya mara moja, huku akitwaa Ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo na mataji la Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ mara mbili.

Namungo FC imethibitisha kumsajili Mchezaji huyo bila kueleza kwa kina amesaini mkataba wa muda gani, lakini taarifa zaidi kuhusu hilo zinatarajiwa kutolewa na Uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Taarifa ya kutambulishwa kwa Nyoni katika Klabu ya Namungo FC imeeleza: #WelcomeTosouthernkillers ?

Tunayofuraha kuwataarifu kuwa Erasto Edward Nyoni amejiunga kuitumikia Timu yetu ya Namungo Fc akitokea Simba SC.

Wakati huo huo Beki wa Kushoto Gadiel Michael ameachwa na Simba SC, ikiwa ni muendelezo wa kutolewa kwa taarifa za wachezaji wanaondoka klabuni hapo katika kipindi hiki cha usajili kuelekea msimu ujao 2023/24.

Simba SC imetangaza kuachana na beki huyo wa zamani wa Klabu za Azam FC na Young Africans leo Ijumaa (Juni 23) Mchana, huku taarifa ya kuachana kwa pande hizo mbili ikieleza: Uongozi wa klabu unapenda kuwajulisha kuwa hatutaendelea kuwa na mlinzi wa kushoto Gadiel Michael baada ya mkataba wake kufikia tamati.

Orlando Pirates kuvuruga mipango ya Nabi
Ifahamu nchi ndogo zaidi duniani