Miamba miwili ya mpira wa kikapu kutoka nchini Malawi imewasili jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya mfululizo wa mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya timu za bigwigs Jogoo, East Zone One, Mbezi na West Zone Three. Mechi hizo zenye hamasa ya aina yake zitachezwa kwenye uwanja Bball Kitaa Park, karibu na Ukumbi wa Gymkhana.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na mratibu wa Bball Kitaa Karabani Karabani pazia la michezo hiyo litafunguliwa kesho ambapo East Zone One watakipiga na Bricks, mchezo unaotabiriwa kuwa ni mgumu na wa kusisimua. Siku hiyo hiyo Mbezi watacheza na Associate Team, mchezo ambao pia unatazamiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Michezo hiyo bado itaendelea kuwateka wakazi wa jiji la Dar es Salaam, ambapo West Zone Three watapambana na Bricks kabla ya Jogoo kuwakaribisha Associate team. “Tuna furaha kubwa kuandaa michezo hii ya kirafiki. Ni moja ya sehemu muhimu katika kudumisha mahusiano, vile vile kuendeleza vipaji vinavyochipukia”, Karabani alisema.

Ujio wa Bricks na Associate teams jijini Dar es Salaam imeonekana si jambo geni baada ya timu za East Zone One na West Zone Three kwenda Malawi mwaka jana. Zikiwa nchini humo, timu hizo zilishinda mechi zao kadhaa.

Karabani ambaye michuano yake ya mpira wa kikapu iko chini ya udhamini wa Sprite, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibua na kukuza vipaji  vya vijana kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo michuano hiyo imekuwa ikifanyika. Vilevile michuano hii inatoa fursa ya kuendeleza ushirikiano baina ya maeneo mbalimbali ya ndani ya nje ya nchi.

“Lengo letu ni kuanzisha michuano ngazi ya kanda mwishoni mwa mwaka huu, ambapo mabingwa kutoka Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe”, Karabani alisema na kuongeza kuwa uzinduzi wa michuano hiyo utafanyika nchini Malawi

Kwa upande wake, Meneja Biashara wa Coca-Cola nchini, Maurice Njowoka alisema anajisikia furaha kubwa kutokana na heshima waliopewa kuisapoti michuano hiyo hapa nchini na kusisitiza kuwa kampuni yake itaendeleza ushirikiano wake na wadau wa mchezo wa kikapu kuzidi kuutangaza mchezo huo.

“Sote tunafahamu kuwa mpira wa kikapu ni moja ya michezo maarufu na yenye nguvu nchini, hasa miongoni mwa vijana ambao wanahitaji aina hii ya msaada ili kuhamasika na kuweza kuendeleza vipaji vyao”, Njowoka alisema.

Picha: Rihanna na Leonardo DiCaprio wakipigana 'Mabusu' zanaswa
Wamiliki wa IPTL wamburuza Zitto mahakamani, wadai alikuwa na 'Maslahi' kwenye Tegeta Escrow