Mchezaji wa mpira wa miguu wa Crystal Palace inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambaye pia ni Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Ufaransa Mamadou Sakho amekubali ombi la Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuwa Balozi wa hiari wa Utalii wa Tanzania, Mamadou amekubali ombi hili wakati alipokutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Betrita Lyimo katika Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.

Mamadou ambaye ni Raia wa Ufaransa amewasili nchini Tanzania Mei 26, 2021 kwa mapumziko ya siku 10 akiwa ameambatana na Familia yake ambapo wametembelea vivutio vya utalii vya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kijiji cha Wamasai cha Seneto, Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro na Visiwa vya Zanzibar.

Timu ya Waandishi wa Habari wa Televishen ya TF1 ya nchini Ufaransa imewasili pia nchini Tanzania tarehe 27/5/2021 kwa lengo la kutengeneza makala maalumu ya ziara ya Mamadou itakayotumika kutangaza Utalii wa Tanzania kwenye Soko la Utalii la Ufaransa hususani maeneo yote ya vivutio vya utalii aliyotembelea.

Aidha, Mamadou amekutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dtk. Hussein Mwinyi, Ikulu Jijini Zanzibar leo Mei 31, 2021.

Dkt. Mwinyi ameipongeza azma ya mchezaji huyo wa klabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza (EPL) ambaye pia ni Mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Mamadou Sakho ya kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi amempongeza Mamadou kwa kuitembelea Zanzibar kwa mara ya pili kutokana na mazingira pamoja na watu wa Zanzibar na utamaduni wao.

Aidha, Dkt. Mwinyi amemueleza mchezaji huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana nae katika kuanzisha kituo hicho cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana Zanzibar na kuwa ujio wake una umuhimu mkubwa katika kuutangaza utalii wa Zanzibar pamoja na vivuto vilivyopo.

Mamadou ambaye amefuatana na Mkewe Majda Sakho, amesema kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo ya kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana Zanzibar kwa kutambua kwamba ana deni na wajibu mkubwa wa kuleta maendeleo Afrika akijuwa kwamba yeye ni Mwafrika licha ya kuwa amezaliwa Ufaransa na anabeba uraia wa Taifa hilo.

Atolewa misumari 30 tumboni
Familia China zaruhusiwa kuzaa watoto watatu