MSIMU huu wa 2015/16 unaonekana kuwa wa historia kwa Yanga, baada ya kufanya mambo ambayo miaka ya hivi karibuni yalikuwa mtihani mzito kwa Wanajangwani hao.

Miongoni mwa mambo hayo ni kitendo cha timu hiyo kuanza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ushindi, wakati misimu iliyopita aidha ilikuwa ikitoka sare au kufungwa kama ilivyokuwa mwaka jana ilipoifuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Tukio la pili ni kitendo cha timu hiyo kuifunga Simba mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo, wakati misimu ya hivi karibuni Yanga ilikuwa ikionewa na Wekundu wa Msimbazi hao kwa kuambulia kipigo au kutoka sare.

Pia kitendo cha Yanga kuifunga Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri wiki chache zilizopita, ni tukio linaloonyesha dalili za timu hiyo kuweka rekodi kwani kila ilipokanyaga kwenye uwanja huo misimu minne iliyopita, ilikuwa ikiambulia kipigo au kupata sare.

Katika mchezo wa msimu huu baina ya timu hizo, Yanga ilishinda mabao 2-0, wakati msimu uliopita kwenye uwanja huo, timu hiyo ililala kwa kipigo kama hicho.

Tukio lingine linaloonyesha huenda msimu huu ukawa wa rekodi kwa Yanga, ni kitendo cha kushinda mechi zote tano za kwanza kwenye Ligi Kuu Bara, wakati kwa misimu ya hivi karibuni haijawahi kuwa hivyo.

 

Muasisi Mwingine Wa Tanu Na CCM Ahamia Chadema, Anamzidi Kingunge
Floyd Mayweather Aendelea Kufanya Kufuru